Rwanda kutenga kambi za dharura kwa wakimbizi wa DRC


 Rwanda imetangaza kuweka kambi za dharura kwa wakimbizi wa DR Congo wanaoendelea kuingia nchini humo wakikimbia kile wanachosema kuwa mauaji dhidi ya wanaozungumza lugha ya Kinyarwanda. Wakimbizi zaidi ya 1200 wako katika kambi hizo kaskazini magharibi mwa Rwanda.

Hatua hiyo inafuatia siku chache tu baada ya Rais wa Rwanda Paul Kagame kutoa wito kwa jumuia ya kimataifa kuwajibika katika sualla la wakimbizi wanaotokana na mzozo wa mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Kambi ya Nkamira katika wilaya ya Rubavu ina wakimbizi zaidi ya 600 wakati kambi ya Kijote umbali wa kilomita 6 kutoka eneo hilo ikihifadhi watu zaidi ya 500.

Waliozungumza na BBC kutoka kambi ya Nkamira wanasema mbali na vita kati ya kundi la M23 na serikali ya DR Congo na makundi mengine ya waasi, katika maeneo wanayotoka, kuna mauaji dhidi ya Watutsi uharibifu wa mali zao ikiwemo mifugo, wakiwahusisha kundi la wapiganaji wa M23.

Mupenzi Nshizirungu alitoka eneo la Kagusa alisema alilazimika kuacha ng’ombe wake baada ya baadhi kukamatwa na kuchinjwa kiholela.

‘’walinikuta nikichunga ng’ombe wangu baada ya kuchinja baadhi ya ng’ombe wengine waliwaua kiholela nikaona heri kuacha ng’ombe na kulinda usalama wangu’’ aliongeza kuwa wametimuliwa katika maeneo yao asilia ‘kwa kuhusishwa na wapiganaji wa M23 wanaoipinga serikali ya DR Congo akisema ‘’ walikuja kutuwinda wakisema sisi ni M23 ‘’ Nshizirungu alisema.

kituo cha afya kimeanzishwa katika kambi hiyo kuwasaidia wakimbizi walioko katika hali mbaya za kiafya na kwamba mashirika ya misaada yanatoa huduma kwa wakimbizi hao.


Kulingana na msemaji wa shirika la wakimbizi UNHCR, Lilly Carlisle , wakiwa katika kambi hizo wakimbizi hao wanapata tu msaada wa dharura kabla ya uwezekano wa kuhamishwa katika kambi nyingine mbali na mpaka wa DRC walikotoka.

Baadhi ya wakimbizi wanasema kambini kuna matatizo Ya malazi na chakula kisichobadilika wakisema tangu walipofika “wanalala kwenye mikeka na kula mahindi kila siku.“

Rwanda inahifadhi wakimbizi wa Congo zaidi ya elfu 72 waliotoroka vita na machafuko mashariki mwa nchi yao tangu zaidi ya miongo miwili iliyopita.Shirika la UNHCR limesema kwamba mwishoni mwa mwezi Novemba wakimbizi takriban 3,000 walikimbilia nchini Rwanda na kuhamishwa katika kambi ya Mahama mashariki mwa nchi hiyo.

Mapema mwezi huu Rais wa Rwanda Paul Kagame alisema nchi yake imechoka kwendelea kubebeshwa mzigo wa matatizo ya Congo.

Rwanda ilisema haina nia ya kuwafukuza au kuwapiga marufuku wakimbizi na kusisitiza , daima inakaribisha watu wanaokimbia ukosefu wa usalama, mateso na vurugu, lakini ikatoa wito kwa Jumuiya ya kimataifa kuchukua jukumu la kutafuta suluhu ya kudumu kwa kundi hilo la wakimbizi kutoka DRC ililotaja kuwa lilisahaulika.

Mvutano kati ya DR Congo na Rwanda umeendelea licha ya juhudi za kidiplomasia kutatua mzozo unaodaiwa kuunga mkono makundi hasimu ya waasi.


Post a Comment

Previous Post Next Post

Nepali Graphics - Learn design, Animation, and Progrmming